Ubelgiji yadumisha hadhi yake dhidi ya Japan, Wamefuzu kucheza robo fainali dhidi ya Brazil.
Kila mmoja amewamiminia sifa wachezaji wa sasa wa kikosi cha Ubelgiji huku wakitabiriwa kuponyoka na Kombe la Dunia 2018.
Japan ilikaribia kuzamisha ndoto na matumaini ya wachezaji hawa, lakini mwisho wa mchezo, Ubelgiji imedhihirisha kwa nini jina lao linawaacha wapinzani wake bila usingizi.
Ubelgiji imekuwa timu ya kwanza kutoka nyuma mabao mawili au zaidi na kushinda mechi hatua za mchujo tangu Ureno kuifunga Jamhuri ya Korea 5-3 ngoma ya robo fainali 1966.
Hii ni baada ya Ubelgiji kuwafikia na kuwafunga Japan licha ya kuachwa nyuma kwa mabao 2-0.
Red Devils walisawazisha na kuondoka na ushindi wa 3-2 dakika za kukunja jamvi na kuwaacha wengi vunywa wazi.
Wakati huo huo, Ubelgiji imedumisha rekodi yake ya kutolazwa kwa kusakata mechi 23 bila kufungwa. (Imeshinda mechi 18 na kutoka sare mechi 5). Mara ya mwisho ilipoteza (0-2) dhidi ya Uhispania mnamo Septemba 2016.
Kabla ya kutemwa, timu nyingine yenye rekodi ndefu ya kutopoteza mechi ilikuwa Uhispania (Imecheza mechi 23 bila kufungwa).
Je, ni nani atakatiza mbio za wachezaji hawa?
Kibarua chao cha kwanza ni dhidi ya Brazil Ijumaa wiki hii, wakati watakuwa na fursa nyingine kuwafunga mdomo wakosoaji wake!