Epstein Files: Jinamizi alilolifuga Trump linavyogeuka kumtafuna

Muda wa kusoma: Dakika 4

Rais wa Marekani Donald Trump anaonekana kushindwa kabisa kukimbia kashfa ya ngono inayomuhusu aliyekuwa rafiki yake Bilionea Jeffyer Epstein – ijulikanayo kama Epstein Files - hata baada ya kuwa nchi ya ugenini, maelfu ya maili kutoka Marekani

Siku ya Jumatatu alipokuwa nchini Uskochi (Scotland) katika ziara ya kikazi na kuhitimisha makubaliano ya biashara na Umoja wa Ulaya, waandishi wa habari wa Uskochi walimuuliza kuhusiana na kashfa hiyo.

Kwa wiki kadhaa sasa, vyombo vya habari vya Marekani vimekuwa vikiibuka na ripoti mpya zinazoonyesha ukaribu aliokuwa nao na Epstein, Bilionea aliyejinyonga Agosti 2019 akiwa katika gereza moja jijini New York alipokuwa akishikiliwa kwa tuhuma za kujihusisha kingono na Watoto nyumbani kwake.

Epstein Files ni jina linalowakilisha nyaraka zilizo na majina na taarifa zingine nyeti za marafiki na washirika wa karibu.

Mafaili yaliyowekwa wazi siku za nyuma yalionyesha baadhi ya marafiki zake walikuwa kama Rais Mstaafu wa Marekani Bill Clinton, Mdogo wa Mfalme wa Uingereza Prince Andrew, Michael Jackson na watu wengine mashuhuri.

Hata hivyo haimaanishi kwamba watu hawa walishiriki pia katika vitendo hivyo vya unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto.

Mazingira ya kujinyonga kwa Epstein yaliibua maswali na dhahania mbalimbali.

Kaka yake Epstein aliibuka na kusema nduguye aliiuwawa, wakati wananchi wengi wakiamini kwamba alishinikizwa kujiua ili kuficha taarifa nyeti na majina ya watu mashuhuri na wenye nguvu serikalini alioshiriki nao katika vitendo vya ngono na watoto.

Mwaka jana mwezi Januari, serikali ya Rais mstaafu Joe Biden iliachilia kurasa zipatazo 1400 za nyaraka ikiwa ni pamoja na safari za ndege za Epstein na majina ya watu kadhaa mashuhuri.

Wakati wa kampeni za uchaguzi, Trump aliahidi kwamba angeweka wazi nyaraka zote zihusianazo na Epstein. Inaonekana aliamini kwamba hatua hii ingewaumiza mahasimu wake

Wafuasi wake walishangilia, na kumsifu kuwa atakuwa rais wa ukweli na uwazi.

Hata hivyo baada ya kuingia madarakani Trump hakuweka wazi nyaraka hizo kama alivyoahidi. Hili halijawafurahisha wafuasi wake, na wameendelea kudai kuwekwa wazi kwa nyaraka hizo.

Mwezi wa pili mwaka huu, wiki chache tu baada ya Trump kuingia madarakani, serikali yake iliachia nyaraka kadhaa za Epstein.

Katika tukio hili, serikali ilialika kundi la 'influensa' kutoka kambi inayomuunga mkono Trump kushuhudia uachiliwaji wa nyaraka zipatazo karatasi 340.

Hata hivyo nyingi ya karatasi zilizoachiwa hazikuwa mpya, zilikuwa zimeachiwa huko nyuma, na nyingine zikiwa na taarifa muhimu zimefutwa futwa.

Hawa 'influensa' hawakufurahishwa – waliona kama serikali inawahadaa tu

Taarifa zilizoibuka hivi karibuni zinasema tangu mwezi May, Trump alijulishwa na Mwanasheria Mkuu wake kwamba jina lake pia lilikuwemo katika nyaraka hizo za Epstein.

Wengi wanahisi inawezekana ikawa sababu kwanini serikali imegoma kuziachia nyaraka hizo.

Gazeti la Wall Street Journal limekuwa mstari wa mbele katika kuripoti taarifa hizi likisema jina la Trump limo katika nyaraka hizo, na kwamba wakati fulani Trump alimtumia Epstein kadi ya kumtakia kheri katika siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwake.

Kadi hii imezua mjadala mkubwa nchini Marekani, huku wengi wakisema ni kielelezo cha urafiki wa ukaribu aliokuwa nao Trump kwa Epstein.

Ikulu ya Whitehouse imegawanyika katika kujibu shutuma hizi. Wakati baadhi ya maofisa wanasema hizo ni habari potofu, wengine wanasema hawawezi kukataa kwamba kweli.

Trump si mgeni wa shutuma zinazohusiana na ngono.

Hivi karibuni kimeibuka kipande cha mahojiano aliyoyafanya Trump na show moja ya radio na mtangazaji Howard Stern. Katika mahojiano hayo, Trump aliulizwa kama naweza kufanya mapenzi na binti wa miaka 24 – akajibu "kabisa, bila wasiwasi"

Mwaka 2005 Trump alirekodiwa bila kujua akijigamba kwamba wanawake humruhusu awafanyie chochote kile kwasababu tu yeye ni mtu maarufu.

Wakati wa muhula wake uliopita, aliibuka dada mmoja anayefanya biashara ya ngono ambaye alimuandama sana Trump kwamba aliwahi kuwa mteja wake.

Mwaka jana mwezi wa pili, kulikuwa na kesi mahakamani iliyohusu taarifa kwamba kuna kipindi Trump alikodi wadada wanaofanya biashara ya ngono, wakojoleane akiwa nao katika chumba chake cha hoteli huko Moscow nchini Urusi.

Wakati mwingine pia Trump anadaiwa kushiriki katika sherehe za ngono huko jijini St Petersburg nchini Urusi.

Hii haimaanishi kwamba Trump mwenyewe alishiriki katika vitendo hivi vya jinai.

Urafiki wa Trump na Epstein

Urafiki wa Trump na Epstein umeanza miaka mingi sana. Kuna picha za tangu miaka ya 90 zikionyesha wawili hawa kuwa pamoja wakati Epstein alipohudhuria harusi ya Trump.

Mwaka 2002, Trump alimuelezea Epstein kama "mtu mzuri sana", baadae Epstein akasema alikuwa rafiki wa karibu wa Trump kwa takribani miaka kumi.

Urafiki wao uliyumba miaka ya 2000, kama miaka miwili tu kabla Epstein hajakamatwa kwa mara ya kwanza kuhusiana na shutuma hizo za ngono.

Wakati ikulu ya Whitehouse inasema Trump alivunja urafiki na Epstein kwasababu ya tabia zake za ajabu ajabu – gazeti la Washington post linasema walipishana kwenye maswala ya biashara ya majengo huko Florida.

Kwanini suala hili limekuwa kubwa?

Wafuasi kindakindaki wa Trump wamekuwa wakiamini kwamba Epstein alikuwa akilindwa na vigogo serikali aliokuwa akishirikiana nao.

Wanagusia namna alivyopewa hukumu ndogo katika kesi yake, na hasa namna alivyoachiwa mazingira yaliyoruhusu ajinyonge akiwa gerezani.

Kwa sehemu Trump alikuza haya madai wakati wa kampeni za uchaguzi wake, akiamini zilikuwa zinamuongezea mtaji wa kisiasa.

Sasa leo hii yupo madarakani, kibao kimemgeukia – jinamizi alilolilisha wakati wa kampeni limemrudia kumtafuna – mafaili haya ya Epstein yanamega umaarufu wake wa kisiasa siku hadi siku.