Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ghislaine Maxwell akutwa na hatia kumsaidia Jeffrey Epstein kuwanyanyasa kingono wasichana
Ghislaine Maxwell amepatikana na hatia ya kuwasajili na kuwasafirisha wasichana wadogo ili kudhulumiwa kingono na marehemu bwenyenye wa Marekani Jeffrey Epstein.
Maxwell mwenye umri wa miaka 60 alipatikana na hatia katika makosa matano kati ya sita aliyokabiliwa nayo - ikiwa ni pamoja na shtaka kubwa zaidi, la ulanguzi wa ngono kwa watoto wadogo.
Uamuzi huo uliafikiwa baada ya siku tano kamili za kujadiliwa na jopo la wanasheria 12 huko New York.
Inamaanisha kuwa sosholaiti huyo wa Uingereza anaweza kutumikia maisha yake yote akiwa jela.
Maxwell hakuonyesha dalili zozote za hisia wakati hukumu hiyo ikisomwa siku ya Jumatano, akimimina tu glasi ya maji ambayo aliivuta mara mbili.
Muda mfupi baada ya uamuzi huo, timu yake ya wanasheria ilisema tayari walikuwa wanashughulikia rufaa.
Teresa Helm, mmoja wa waliomshtumu Jeffrey Epstein, aliwasifu wanawake waliotoa ushahidi wakati wa kesi hiyo.
"Haki inaongoza leo," aliiambia BBC. "Nimejawa na shukrani kwa kila mtu jasiri, shujaa na anayeendeshwa na haki ambaye amepigania matokeo haya.
"Ghislaine Maxwell hatakuwa tena na fursa ya kuchukua chochote kutoka kwa mtu yeyote. Atakaa upande mwingine wa uhuru."
Maxwell alipatikana na hatia ya:
• Ulanguzi wa ngono wa watoto wadogo, ambao una adhabu ya juu zaidi ya miaka 40 jela
• Kusafirisha watoto wadogo kwa nia ya kushiriki katika shughuli za ngono za uhalifu, ambayo huchukua kifungo cha juu cha miaka 10
• Kula njama ya kusafirisha watoto kwa nia ya kushiriki katika shughuli za ngono za uhalifu, ambayo huchukua kifungo cha juu cha miaka mitano.
• Kula njama ya kuwashawishi watoto kusafiri ili kushiriki katika vitendo vya ngono haramu, ambayo inaweza kuwa na kifungo cha juu cha miaka mitano.
• Kula njama ya kufanya biashara haramu ya ngono ya watoto, ambayo pia ina adhabu ya juu zaidi ya miaka mitano
Hakupatikana na hatia ya kosa moja - kumshawishi mtoto kusafiri ili kushiriki katika vitendo vya ngono haramu.
Mwanasheria wa Marekani Damian Williams alikaribisha uamuzi huo na kupongeza "ushujaa" wa waathiriwa waliojitokeza.
"Baraza la majaji kwa kauli moja limempata Ghislaine Maxwell na hatia ya uhalifu mbaya zaidi unaoweza kufikiria - kuwezesha na kushiriki katika unyanyasaji wa kingono kwa watoto," taarifa hiyo ilisema
Hakuna pa kukimbilia
Mara ya kwanza nilipomwona Ghislaine Maxwell, nilimfuata kwenye mitaa ya Manhattan, nikimuuliza kuhusu madai ya kutisha dhidi yake.
Muongo mmoja baadaye, nilimwona kwa mara ya mwisho, kortini na sikuweza tena kutoroka ukweli kuhusu maisha yake na Jeffrey Epstein.
Sakata hii ya biashara ya ngono haikuwa kwa ajili ya faida bali ni kwa ajili ya kuwafurahisha 'wagonjwa' hao wawili wenye ushawishi
Wawili hao walisimamia kundi la kijamii lenye ushawishi na mara nyingi marafiki wao waliotajwa majina katika maeneo ya juu kama vile Bill Clinton, Donald Trump au Prince Andrew. Hilo liliwavutia wahasiriwa wao, wakivutwa na zawadi na ahadi za kuwasaidia kazi zao na shule.
Waendesha mashtaka walisema mchakato wa "kuwalea" wasichana wachanga kwa unyanyasaji ulikuwa sehemu muhimu ya "mbinu " za Maxwell.
Utajiri wao na kujulikana pia ilikuwa muhimu kwa njia nyingine - waliwatisha na kuwanyamazisha wahasiriwa wao na kuwakinga wawili hao wasichunguzwe.
Maxwell, mshirika wa muda mrefu wa mtuhumiwa wa kosa la kushiriki ngono na watoto aliyepatikana na hatia Epstein, amekuwa gerezani tangu kukamatwa kwake Julai iliyopita.
Epstein alijiua mnamo 2019 wakati akingojea kesi nyingine kuhusiananna uhalifu wa kingono
Sosholaiti aliyefahamika vizuri, inasemekana alimtambulisha Epstein kwa watu matajiri na wenye nguvu ikiwa ni pamoja na Bill Clinton na Prince Andrew.
Wakati wa kesi hiyo iliyochukua mwezi mzima, mawakili wa Maxwell walidai kwamba alikuwa kafara wa Epstein wakati waendesha mashtaka walitaka kuwaunganisha wawili hao kama "washirika wa uhalifu" ambao waliendesha "mpango wa piramidi ya unyanyasaji".
Wanawake wanne walisimama kwenye kesi hiyo. Wote walisema walikuwa wamenyanyaswa kingono na Epstein kabla ya kutimiza umri wa miaka 18, na kwamba Maxwell alikuwa amewahimiza, kuwezesha na hata kushiriki katika ngono.
Mwanamke mmoja tu, Annie Farmer, alitumia jina lake halisi katika ushuhuda wake, huku wengine wakitumia majina bandia kulinda utambulisho wao.
"Ghislaine Maxwell alifanya maamuzi yake mwenyewe. Alifanya uhalifu akiwa ameshikana mkono na Jeffrey Epstein. Alikuwa mwanamke mzima ambaye alijua hasa alichokuwa akifanya," Mwanasheria Msaidizi wa Marekani Alison Moe alisema.
Bado haijabainika ni lini Maxwell atahukumiwa.