Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mwanamfalme Andrew na Bill Clinton watajwa katika nyaraka za myanyasaji wa kingono Jeffrey Epstein
- Author, Max Matza & Bernd Debusmann Jr
- Nafasi, BBC News
Bill Clinton na Mwanamfalme Andrew wametajwa katika nyaraka za mahakama za watu wanaohusishwa na bilionea na myanyasaji wa kingono Jeffrey Epstein.
Jaji wa mahakama ya shirikisho huko New York ameamuru kutolewa kwa nyaraka hizo kama sehemu ya kesi inayomhusisha mshirika wa Epstein, Ghislaine Maxwell.
Maxwell anatumikia kifungo cha miaka 20 jela kwa uhalifu alioufanya na Epstein.
BBC imepitia nyaraka hizo zenye kurasa 943, zilizotolewa Jumatano jioni. Baadhi ya waliotajwa wanatuhumiwa kwa makosa, wengine kwenye orodha hiyo ni watoa tuhuma na mashahidi watarajiwa.
Alipoamuru orodha hiyo iwekwe hadharani, Jaji wa New York, Loretta Preska alisema wengi wa wale waliotajwa katika orodha hiyo tayari wametambuliwa na vyombo vya habari au katika kesi ya jinai ya Maxwell.
Aliongeza kuwa wengi wa waliotajwa hawakuleta pingamizi la kutolewa kwa nyaraka hizo.
Nyaraka hizo zinamtaja Johanna Sjoberg, aliedai kwamba Mwanamfalme Andrew alipapasa matiti yake wakati ameketi kwenye kochi ndani ya nyumba ya Epstein huko Manhattan mwaka 2001.
Jumba la Buckingham hapo awali lilisema madai yake "si ya kweli kabisa."
Bi Sjoberg alidai Prince Andrew aliweka mkono wake kwenye kifua chake ili kupiga picha na mshtaki mwingine, Virginia Giuffre.
Mwaka 2022, mfalme wa Uingereza alilipa mamilioni ya dola kwa Bi Giuffre ili kutatua kesi aliyowasilisha akidai alimnyanyasa kingono alipokuwa na umri wa miaka 17.
Mwanamfalme Andrew alisema hajawahi kukutana na Giuffre na akakana madai yake.
Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton pia ametajwa katika nyaraka za mahakama, ingawa hakuna tuhuma zozote dhidi yake. Alipotafutwa kwa maoni, wasaidizi wake walirejelea taarifa aliyotoa 2019 akisema "hajui chochote" juu ya uhalifu wa Epstein.
Kulingana na nyaraka hizo, Sjoberg anasema Epstein aliwahi kumwambia kuwa Bill Clinton anapenda wasichana. Clinton alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mfanyakazi wa ndani wa White House mwenye umri wa miaka 22 alipokuwa rais wa Marekani.
Nyaraka hizo ni pamoja na ushuhuda kutoka kwa Maxwell akithibitisha Clinton alisafiri kwa ndege binafsi ya Epstein, lakini hakujua ni mara ngapi.
Clinton alisafiri kwa ndege ya Epstein katika safari za kiutu barani Afrika mapema 2000 na wakati huo alimsifu Epstein kama mfadhili aliyejitolea, ingawa baadaye alisema alikata uhusiano naye.
Taarifa ya Clinton ya 2019 ilisema aliandamana kwenye safari zake ndani ya ndege ya Epstein, akiwa na wafanyakazi na wafadhili kutoka shirika lake la hisani, Clinton Foundation.
"Walinzi wa Rais (Secret Service) walisafiri naye katika kila safari," taarifa hiyo ilisema.
Nyaraka hizo za mahakama zinaeleza juhudi za wakili wa Maxwell kukanusha ripoti za vyombo vya habari - kwamba muda mfupi baada Clinton kuondoka ofisini, alisafiri kwenda katika kisiwa binafsi cha Epstein huko Caribbean.
Wakili wa Maxwell alisema rais huyo wa zamani wa Marekani "hakusafiri, wala hakuwepo katika kisiwa cha Little St James kati ya Januari 1, 2001 na Januari 1, 2003."
Wakili huyo aliongeza iwapo madai hayo ni ya kweli, walinzi wa rais wangetakiwa kuwasilisha kumbukumbu za safari.
Nyaraka hiyo pia inajumuisha ushuhuda kutoka kwa Sjoberg akisema Epstein alimwambia atawasiliana na Donald Trump wakati wakielekea kwenye moja ya kasino zake huko New Jersey.
"Jeffrey alisema, 'Sawa, tutampigia Trump," alitoa ushahidi, baada ya marubani kusema ndege haiwezi kutua New York na ingepaswa kutua katika Jiji la Atlantic, New Jersey.
Nyaraka hizo hazina tuhuma dhidi ya Trump. Sjoberg anaulizwa wakati mmoja katika uwasilishaji kama aliwahi kuwasiliana na Trump, na anajibu: "Hapana."
Alfredo Rodriguez, mfanyakazi wa nyumbani ambaye alipewa jukumu la ulinzi wa Epstein, alimwelezea Maxwell kama "bosi" katika ushahidi wake.
Rodriguez, aliyefariki mwaka 2015, kila wakati aliambiwa abebe pesa ili kuwapa wasichana wa sekondari, na wasichana ambao walikuwa wakimsaidia Epstein kuajiri, nyaraka zinasema.
Epstein alifariki gerezani mwaka 2019 - alipokuwa akingojea mashtaka ya biashara ya ngono. Mchunguzi wa matibabu wa New York alisema kifo hicho kilitokana na kujiuwa.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Esther Namuhisa