Kwenda haja kubwa mara tu baada ya kula kunaashiria ugonjwa?

Muda wa kusoma: Dakika 5

Hitaji la kwenda chooni dakika chache tu baada ya kula ni tatizo ambalo watu wengi hukabiliana nalo kila siku.

Hili pia linaibua swali akilini, je, chakula tulichokula kimemeng'enywa ipasavyo?

Kulingana na wataalamu wa matibabu, moja ya sababu za haya ni kula kiasi kidogo wakati wa kazi na kula vitu vingi unavyopenda wakati wa likizo.

Lakini swali ni, je, ni kawaida kujisaidia haja kubwa mara baada ya kula au ni ishara ya ugonjwa? Au kwenda chooni mara kadhaa kwa siku ni tatizo au la?

Unaweza kusoma

Hapa utapata jibu la maswali haya kwa msaada wa wataalamu wa matibabu na utafiti.

Daktari bingwa wa magonjwa ya utumbo, Dkt. Mahadevan, anasema, "hitaji la kwenda chooni mara baada ya kula chakula inaitwa 'gastrocolic reflex'. Lakini watu wengi wana dhana potofu kwamba chakula kinacholiwa mara moja huwa kinyesi? Ilhali sivyo."

Je, chakula tunachokula hubadilika kuwa kinyesi kwa haraka?

Kulingana na utafiti, kwa kawaida huchukua saa 10 hadi 73 kwa chakula kutoka mwilini kama kinyesi. Hii inaitwa 'muda wa kusafirisha chakula'.

Hata hivyo, wakati huu unategemea mambo mengi, kama vile umri wa mtu, jinsia, uzito na lishe.

Chakula kinapofika tumboni, neva hutuma ishara kwenye utumbo mpana. Ishara hizi huuambia utumbo mpana kusinyaa, na kusukuma kinyesi kilichopo awali kuelekea kwenye rektamu. Hii huongeza hitaji la kujisaidia haja kubwa.

Kinyesi kinapopita kwenye rektamu kupitia utumbo mpana, nafasi kwenye utumbo mpana huondolewa, ambayo husababisha uwezo wa kusaga chakula kuongezeka zaidi. Mchakato huu huitwa 'gastrocolic reflex'.

Dkt. Mahadevan anasema, "Hiki ni kitendo cha kawaida cha mwili, ambao huonekana zaidi kwa watoto wadogo. Kwa sababu hii, mara nyingi watoto wadogo hujisaidia haja kubwa mara tu wanapokunywa maziwa.

Inaweza kuhisiwa ndani ya dakika chache hadi saa moja baada ya kula. Kulingana na utafiti, mchakato huu ni wa haraka zaidi kwa watoto wadogo, huku ukiwa polepole zaidi kwa watu wazima.

Dkt. Mahadevan anaelezea kwamba ni kawaida kuhisi hivi, lakini ikiwa hali hii haitadhibitiwa au ni kali sana, basi inaweza kuwa ishara ya tatizo la tumbo au ugonjwa wa utumbo.

Dkt. Mahadevan anaongeza zaidi kwamba 'matatizo ya utumbo yanayosababisha maumivu', ni tatizo kubwa la utumbo, lakini linaweza kuzuiwa.

Dalili kuu ni zipi?

Kulingana na Huduma ya Kitaifa ya Afya ya Uingereza, ugonjwa wa mfumo wa mmeng'enyo wa chakula dalili zake kuu ni:

• Maumivu ya tumbo , ambayo kwa kawaida huhusishwa na haja ya kwenda chooni

- Gesi nyingi na uvimbe

• Kuhara, kuvimbiwa, au vyote viwili

• Kuhisi kwamba tumbo halijasafishwa kabisa hata baada ya kwenda chooni

Kulingana na ushauri wa Huduma ya Kitaifa ya Afya, ikiwa dalili hizi zitaendelea kwa zaidi ya wiki 4, basi hakika wasiliana na daktari.

Hakuna sababu dhahiri ya tatizo hili, lakini mambo yafuatayo ambayo yanaweza kusababisha ugonjwa wa mfumo wa mmeng'enyo wa chakula ni;

•Mvinyo

• Kafeini (katika chai na kahawa)

• Chakula chenye viungo au mafuta

• Msongo wa mawazo na wasiwasi

• Matumizi ya mara kwa mara ya viuavijisumu (antibiotics)

Tatizo la mfumo wa kumeng'enya chakula linaweza kusababisha matatizo mengine sambamba na hitaji la kwenda chooni baada ya kula:

• Matatizo ya gesi

• Uchovu na ukosefu wa nguvu

•kuhisi mgonjwa

• Maumivu ya mgongo

• Hamu ya mara kwa mara ya kwenda haja ndogo

• Kuhisi kama haja ndogo haijatoka yote baada ya kujisaidia

Kulingana na utafiti, asilimia 5 hadi 10 ya idadi ya watu duniani wana ugonjwa wa mfumo wa kumeng'enya chakula. Mtu mmoja kati ya kila watu watatu wenye IBS pia ana wasiwasi au mfadhaiko.

Arun Kumar, daktari na mtaalamu wa lishe anasema, "IBS hutokea kwa watu wengi. Licha ya kuwa na afya njema kimwili. Kuna aina mbili kuu, IBS-C, ambayo huambatana na kuvimbiwa na maumivu ya tumbo, na IBS-D, ambayo hujulikana kwa kuhara pamoja na usumbufu."

Dkt. Mahadevan anasema, "Dalili za ugonjwa huu zinaweza kudhibitiwa kwa kufanya mabadiliko katika lishe na mtindo wa maisha, na kutumia mbinu za kudhibiti msongo wa mawazo. Ikiwa dalili ni kali, ni vyema kushauriana na daktari au kutafuta matibabu."

Daktari bingwa wa magonjwa ya njia ya utumbo Dkt. Ravindran Kumaran anasema, "Baadhi ya watu wana tabia ya kwenda chooni mara tu baada ya kula chakula kwa miaka mingi. Ikiwa haiwasababishii matatizo yoyote ya kimwili au kiakili, basi haya si matatizo.

Lakini ikiwa ghafla, hamu kubwa kama hiyo itaanza kuibuka na kuendelea, ni muhimu kuizingatia."

Dkt. Ravindran Kumaran anasema, "Watu wanaokwenda ofisini au shuleni na chuo kikuu kila siku wanaweza kuona ni vigumu kwenda chooni tena na tena.

Wakiwasiliana nasi, tunapendekeza mabadiliko fulani ya mtindo wa maisha. Vinginevyo, hakuna sheria maalum ya mara ngapi mtu anapaswa kujisaidia haja kubwa kwa siku. Ikiwa kuna kuvimbiwa au kuhara mara kwa mara, basi daktari anapaswa kushauri.

Akisisitiza hili, Dkt. Mahadevan anasema, "Unapoona mabadiliko ya mara kwa mara katika tabia yako ya kawaida ya kujisaidia haja kubwa, usipuuze. Kwa mfano, kuamka ili kujisaidia haja kubwa mara kwa mara usiku kunaweza kuwa mabadiliko hatari. Inaweza pia kuwa dalili ya ugonjwa mwingine."

"Vitu vinavyonata kwenye kinyesi (kamasi inayoweza kuonekana nyeupe) au kutokwa na damu, kupungua uzito, kuvimbiwa mara kwa mara au kuhara kunaweza kuwa dalili za magonjwa ya utumbo. Ni vyema kushauriwa na daktari kwa hili."