Je, watu wanapaswa kupunguza kula wali?

Muda wa kusoma: Dakika 5

Kwa zaidi ya nusu ya idadi ya watu duniani, mchele ndio chakula chao cha kila siku na ni ishara ya utamaduni, mila, na mapambano ya kimaisha.

Adrian Bianca Villanova, msikilizaji wa BBC kutoka Manila, mji mkuu wa Ufilipino, anasema "mchele sio tu bidhaa ya chakula, ni ishara na nembo ya utamaduni. Wafilipino wengi hula wali mara tatu kwa siku, kifungua kinywa, chakula cha mchana na chakula cha jioni”.

Lakini kadiri shinikizo la mabadiliko ya tabia nchi linavyoongezeka, swali linazuka: Je, watu wanapaswa kupunguza kula wali?

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa linasema kuna aina zaidi ya 50,000 za mimea inayoliwa, na mimea 15 tu ndio hutoa 90% chakula kinacholiwa na idadi kubwa ya watu duniani. Mchele, ngano, na mahindi, inaongoza katika orodha.

Kati ya asilimia 50 na 56 ya watu ulimwenguni hutumia wali kama chakula chao kikuu,” anasema Dakt. Ivan Pinto, mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mchele Ulimwenguni. Hii ina maana wali ni chakula kikuu cha kila siku cha watu wapatao bilioni nne duniani.

Mpunga hulimwa sana Kusini na Kusini-mashariki mwa Asia, na pia unatumika sana barani Afrika, na aina mbali mbali za mpunga hulimwa Ulaya na Amerika Kusini. Lakini mpunga kama chakula kikuu duniani, huzalishwa kwa gharama kubwa.

Pia unaweza kusoma

Unahitaji maji mengi

Mmea wa mpunga unahitaji maji mengi," anasema Jean-Philippe Laborde, mkurugenzi wa Tilda, kampuni ya kuzalisha mchele yenye makao yake makuu nchini Uingereza, chini ya kampuni ya kimataifa ya Ebro Foods ya Uhispania.

"Inachukua kati ya lita 3,000 na 5,000 za maji kukuza kila kilo ya mchele, na hicho ni kiasi kikubwa."

Uzalishaji mwingi wa mpunga hufanyika katika mashamba yaliyofurika maji, haswa Kusini na Kusini-mashariki mwa Asia. Njia hii ya kukuza mpunga hupunguza kiasi cha oksijeni katika mazingira.

"Mashamba yanapokuwa na maji mengi, vijidudu huzalishwa ambavyo hutoa kiasi kikubwa cha gesi ya methane," anasema Dk. Ivan Pinto.

Kulingana na Shirika la Kimataifa la Nishati, methane ni gesi chafu inayohusika kwa karibu 30% ya ongezeko la joto duniani.

Taasisi ya Utafiti wa Mchele Duniani inakadiria kuwa uzalishaji wa mpunga unachangia 10% ya uzalishaji wa gesi chafu katika sekta ya kilimo duniani kote.

Ukulima bora

Tilda imebuni njia mpya ya umwagiliaji, ambapo bomba huzikwa sentimeta 15 ndani ya ardhi. Badala ya shamba kufunikwa na maji, wakulima humwagilia wakati hakuna maji kwa kipindi fulani.

"Kwa kawaida, kuna mizunguko 25 ya umwagiliaji kwa kila kipindi cha ukulima, lakini kwa kutumia njia ya umwagiliaji ya namna hii, unaweza kupunguza idadi hiyo hadi mizunguko 20. Kwa kupunguza mzunguko wa umwagiliaji, unaweza kuzuia uzalishaji wa gesi ya methane," anasema Laborde.

Mwaka 2024, Tilda ilipanua mradi wake wa majaribio wa umwagiliaji kutoka kwa wakulima 50 hadi wakulima 1,268, na matokeo yalikuwa ya kushangaza.

"Tuliweza kupunguza matumizi ya maji kwa 27%, matumizi ya umeme kwa 28%, na matumizi ya mbolea kwa 25%," anasema Laborde, akibainisha kuwa mavuno yaliongezeka kwa takriban 7% katika kipindi hiki.

Laborde anabainisha kuwa viwango vya methane pia vilipungua kwa 45%, na anaamini kupunguza zaidi mzunguko wa umwagiliaji, kutapunguza uzalishaji wa methane kwa 70%.

Aina mpya ya mpunga

Ingawa mchele ni chakula cha mabilioni ya watu duniani kote, lakini mabadiliko ya hali ya hewa ya sasa yanatishia uzalishaji wake huku maeneo yanayolima mpunga duniani kote yakikabiliwa na joto kali, ukame, na mvua kubwa na mafuriko.

Mwaka 2024, wakati wa msimu wa kilimo cha mpunga nchini India, joto lilifikia nyuzi joto 53. Nchini Bangladesh, mafuriko makubwa yaliharibu mazao yote.

Taasisi ya Utafiti wa Mchele Duniani imetafuta suluhisho. Mfano mmoja wa kuvutia ni aina ya punga, unaoweza kukaa chini ya maji kwa siku 21.

"Aina hizi hustahimili mazingira ya mafuriko na huishi bila kuharibika hadi mafuriko yanapopungua," anasema Pinto, akiongeza kuwa aina hii ya mpunga imekuwa maarufu sana katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko nchini Bangladesh.

Chaguo jingine?

Baadhi ya serikali zinajaribu kuhimiza watu kula vyakula vingine mbali na wali. Nchini Bangladesh, miaka 15 iliyopita, kulikuwa na kampeni ya kuwahimiza watu kutumia viazi baada ya bei ya mchele kupanda.

China ilichukua hatua kama hiyo 2015, ikitangaza viazi kama chakula bora na chenye lishe. Nchi hiyo ikawa mzalishaji mkubwa wa viazi, na katika maeneo mengi ya nchi, watu walianza kula viazi kama chakula chao kikuu, lakini kampeni ilishindwa.

"Kusini-magharibi na kaskazini-magharibi mwa China, viazi hutumiwa kama chakula kikuu," anasema Jacob Klein, mtaalamu wa masuala ya kijamii na tamaduni katika Chuo Kikuu cha Sussex huko London.

Lakini anasema katika maeneo mengi kula viazi ni dalili ya umaskini.

Anasema watu wa kusini-magharibi mwa China wakikwambia nakula viazi, wanamaanisha, "niko katika umaskini." Kuna unyanyapaa na sifa mbaya miongoni mwa watu kuhusu kula viazi.

Mchele una jukumu kubwa katika maisha ya watu ulimwenguni kote. Ni mtamu, ni rahisi kupika, na ni rahisi kusafirisha na kuhifadhi. Ulimwengu hutumia takriban tani milioni 520 za mchele kila mwaka.

Adrian Bianca Villanova, kutoka Ufilipino, anasema anaweza kupunguza kula wali, lakini ni vigumu kuacha kabisa.

“Hata nikiamua kuacha kula wali, kila nikienda kwenye sherehe au nyumba za watu wengine nitakuta wali. Nadhani natakiwa kula wali kidogo, lakini siwezi kuacha kabisa kwa sababu ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku."