Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kombe la Dunia: Didier Deschamps asema ushindi wa Ufaransa ni miujiza
Ubingwa wa Ufaransa ni wa ''kutoka kwa mungu'' baada ya "uchungu" wa kupoteza fainali ya mataifa bora Ulaya 2016, alisema kocha wake Didier Deschamps.
Walipoteza 1-0 dhidi ya Ureno fainali ya Euro 2016, wakiwa wenyeji.
Les Bleus iliilaza Croatia 4-2 Moscow siku ya Jumapili na kuwa mabingwa wa dunia kwa mara ya pili katika historia yao.
"Ni wachezaji wadogo, walioko juu ya mataifa yote katika dunia. Wengine ni mabingwa wakiwa na miaka 19," alifunguka Deschamps, nahodha wa Ufaransa waliponyakua ubingwa 1998.
Alisema ushindi huo "haukumhusu yeye ", akiongeza: "Ni wachezaji walioshinda mechi."
Deschamps anahisi timu yake "ilistahili ushindi wake".
"Hatukucheza mchezo maridadi vile lakini tumeonyesha ukomavu na ubora wa kiakili," aliongeza.
"Licha ya yote, tumefunga mabao manne.
"Ndani ya siku 55, tumefanya kazi nyingi. Tunajivunia kuwa Wafaransa,kuwa Bleus.
"Kikosi hiki kiliweka bidii na tumepitia kipindi kigumu katika safari yetu. Iliuma sana kupoteza Kombe la mataifa bingwa wa bara Ulaya miaka miwili iliyopita, lakini pia tumejifunza mengi."
Mfungaji wa goli la Ufaransa la Penalti, Antoine Griezmann alisema "tuliweza kuleta mabadiliko" licha ya Croatia kuingia mechi ikiwa na nguvu kuwashinda.
"Sifahamu niko wapi!" alisema mwisho wa mechi. "Niko na furaha sana. Haikuwa mechi rahisi."
Wakati huo huo, Meneja wa Croatia Zlatko Dalic ameweka hisia zake kuhusu uamuzi wa kutoa penalti kwa Ufaransa "tusiondoe kutoka sababu za ushindi wa Ufaransa". Alisema.
Lakini aliongeza, "Hufai kupeana penalti kama hiyo" fainali ya Kombe la Dunia.
"Tukiangalia bahati katika Kombe hili, kwa kweli leo, bahati haikuwa nasi tukizungumzia magoli mawili ya kwanza tuliyolishwa," alieleza Dalic.
"Bao la kwanza lilikuwa la kujifunga ingawa tulitawala mechi bila lango letu kuvamiwa. Tulisawazisha na wachezaji wetu kumakinika, kisha mkwaju wa penalti ukatuandama na kwenda dhidi yetu.
"Namheshimu mwamuzi na alichukua msimamo kulingana na aliyoshuhudia. Simaanishi kuwa na mtazamo hasi."
Dalic aliongoza kuwa VAR "ni muhimu kwa soka" lakini "uamuzi ukiwa ni dhidi yako, ni mbaya".
Kocha huyo mwenye miaka 51 aliongeza: "Kwa miezi kadhaa, mimi na kikosi changu tulitia bidi sana. Limependeza kufanya kazi na nyota hawa na ninafurahia muda tuliofanya kazi pamoja.
"Nitachukua mapumziko. Siwezi kufanya uamuzi wa kushtukizia. Kwa sasa siwazi kuhusu jambo lolote isipokuwa kutua Croatia na kupumzika."
Nahodha wa Croatia Luka Modric, aliyepokea mpira wa dhahabu kwa kuwa mchezaji bora wa Kombe la Dunia, alisema timu yake "haina majuto hata kidogo".
Alihisi walikuwa "timu bora kwa kipindi kirefu mechini".
"Kwa bahati mbaya, mabao ya kipuzi yaliishia kimiani na kuvuta ushindi kwao," alisema Modric.
"Wanasherekea lakini pia sisi tunajivunia.
"Hisia hizi zikitulia na kumalizika, tutaweza kutathmini na kujua tulipokosea."
Na kuhusu kutuzwa 'Golden Ball' aliongeza: "Najivunia kunyakua tuzo hili. Upendo usiosahaulika wa mashabiki pia inanipa furaha zaidi.
"Unaondoka ukijua kwamba licha ya kufungwa ,umetimiza mafaniko makubwa,lakini inauma ukitambua kuwa ulikwama baada ya kubakisha tu kidogo kukaribia ubingwa."