Dunia inasheherekea mwaka mpya wa 2026, sherehe zikianza kwa kutofautiana muda. Sherehe za kuukaribisha mwaka mpya zilianza katika baadhi ya maeneo ya dunia, huku mataifa ya Pasifiki yakiongoza kuingia mwaka 2026 kabla ya sehemu nyingine za dunia. Miji na visiwa kadhaa tayari vimebadilisha kalenda, vimeshaingia mwaka 2026, huku mamilioni ya watu wakishuhudia fataki, sherehe za kitamaduni na mikusanyiko ya kifamilia kuashiria mwanzo wa mwaka mpya.
Jiji la Sydney nchini Australia lilikuwa miongoni mwa maeneo ya kwanza yenye watu wengi kuukaribisha mwaka mpya kwa onyesho kubwa la fataki lililopamba anga la Bandari ya Sydney.
Mamia ya maelfu ya watu walikusanyika kushuhudia tukio hilo, ingawa furaha ilichanganyika na huzuni, baada ya tukio la shambulio lililotokea Bondi Beach mapema mwezi huu, lililoacha majonzi kwa wakazi wa jiji hilo.
Sherehe pia zikafuatwa katika mataifa jirani ya Pasifiki ikiwemo Fiji, Tonga na Samoa, ambapo wakaazi walikusanyika kwa sala, ngoma za kitamaduni na fataki ndogo ndogo. Wakati huohuo, Kisiwa cha Chatham cha New Zealand, kilicho mbali na bara hilo, kiliingia mwaka 2026 dakika 15 tu baada ya Kiritimati, kikifuata ratiba yake maalum ya muda.
Kwa upande wa kipekee, mfamasia mmoja kutoka Uingereza tayari ameukaribisha mwaka mpya akiwa Samoa, kabla ya kusafiri kwenda American Samoa, eneo ambalo lina saa tofauti, ili kuukaribisha tena mwaka mpya mara ya pilli, kitendo anachokielezea kama “kusafiri kwenye muda”.
Mataifa mbalimbali yakafuata kama China, Singapore, Ufilipino, Japan na Korea Kusini, ambako kulifanyika hafla za kupigwa kwa kengele katika miji ya Tokyo na Seoul.
Baada ya hapo, New Zealand ilifuata kwa kuukaribisha mwaka mpya kwa sherehe za fataki (fireworks) katika jiji la Auckland.
Kadri saa zinavyoendelea kusogea, mataifa mengine duniani yameendelea kuupokea mwaka mpya ikiwemo ya Afrika, Ulaya na hatimaye Amerika yanayopokea mwaka mpya kwa kuchelewa kidogo