Uongozi: Komedi, Muziki, Filamu,Warembo, wanasoka kutawala katika siasa

    • Author, NA MARKUS MPANGALA
    • Nafasi, Mchambuzi

Mabadiliko makubwa duniani yametokea katika mfumo mzima wa siasa na demokrasia. Wakati ulimwengu ukiwa umeonyesha kupoteza ladha ya wanasiasa na viongozi wenye sifa, uwezo na karama ya uongozi ambao wametokana na mfumo wa kisiasa uliozoeleka, yameibuka makundi mengine ambayo limekwenda kinyume cha mazoea yaliyokuwepo.

Kuibuka kwa wachekeshaji,wanamuziki,wacheza filamu,wanasoka na wanamitindo wenye mvuto, ushawishi, nguvu, uwezo na kukubalika katika siasa na uongozi kumewatikisa wanasiasa waliopitia ukada wa vyama.

Ulimwengu mpya wa teknolojia umechangia kiasi kikubwa wanamuziki,wachekeshaji,wanamitindo,wanasoka na wacheza filamu kuongeza ushawishi,nguvu na kukubalika miongoni mwa wananchi hivyo kuwalazimisha kujiingiza kwenye siasa.

Baadhi ya mataifa yakiwemo Marekani yamewahi kuongozwa na rais aliyekuwa mchezaji mwigziaji wa filamu huko Hollywood, Ronald Reagan.

Ulimwengu wa tatu umeshuhudia kuibuka kwa kundi la waburudishaji kuziteka siasa, kwakuwa wanawafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii hali ambayo inawavutia watu mbalimbali kuona busara,uwezo,nguvu na ushawishi ambao unafaa kuingizwa kwenye uongozi katika ngazi mbalimbali.

Burudani na michezo imezidi kuwa gumzo kote duniani ambapo wanamichezo wamezidi kujizoela umaarufu na kuchaguliwa kuongoza mataifa yao kama vile ilivyokuwa kwa Goerge Opong Weah aliyechaguliwa kuwa rais wa Liberia. Wakati Weah akichaguliwa, mwanasoka wa zamani wa Senegal, El Hadji Diouf alibainisha nia yake ya kuwa kiongozi miaka ijayo.

Kwa muktadha huo ukiacha kundi la kwanza la burudani na michezo, lipo kundi jingine ambalo linawahusiaha viongozi ambao kwa hakika hawakuwa sehemu au wapo nje ya mfumo wa kisiasa, lakini wakapata

Wanasiasa na viongozi watata

Hili ni kundi la kwanza la viongozi ambao wametoka nje ya mnyororo wa mfumo wa kisiasa. Hawa ni viongozi ambao wameingia kwenye siasa bila kubebwa na mfumo wa kisiasa wa nchi husika, badala yake wamejijenga wenyewe na kuibuka kuwa wanasiasa mahiri wanaopendwa na wapigakura sehemu mbalimbali duniani.

Napenda kuhitimisha kuwa kundi hili linajumuisha wanasiasa watata ambao hulka na mienendo yao imekuwa ikitibua mambo na kuwatisha wanasiasa waliozoea kubebwa na mfumo wa wakati wote.

Katika kundi hili wamo viongozi kama Rais wa Marekani, Donald Trump, mwanasiasa Julius Malema (Kiongozi wa chama cha EFF Afrika kusini), John Magufuli (Tanzania), Marie Le Pen (Mwanasiasa mwenye kupendelea ubaguzi wa Ufaransa na kujitenga Jumuiya ya Ulaya). Ingawa Marie Le Pen hakushinda urais wa Ufaransa, lakini ni mwanasiasa anayebeba alama zote za vioongozi watata waliopata kutokea duniani.

Waburudishaji na wanamichezo

Kundi la pili wamo Waziri mkuu wa Pakistan, Imran Khan ambaye alikuwa mchezaji wa mchezo wa Kriketi, George Opong Weah ni rais wa Liberia ambaye amewahi kuwa mchezaji bora wa dunia,Afrika na mwanasoka aliyezichezea klabu maarufu duniani kama AS Monaco, AC Milan na Chelsea.

Mwingine ni Jimmy Morale ambaye ni mchekeshaji yaani Komedi aliyeshinda uchaguzi wa rais nchini Guatemala. Naye Ronald Reagan alikuwa mcheza sinema maarufu wa Hollywood ambaye aliukwaa urais wa Marekani.

Tanzania: Nchini Tanzania wamo wanamichezo na waburudishaji kama vile Joseph Mbilinyi (Sugu), Joseph Haule (Profesa Jay), ambao wameshinda uchaguzi katika nafasi ya ubunge wa Mbeya Mjini na Mikumi kupitia Chadema. Wanamitindo Jokate Mwegelo (Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe na kada wa CCM), Crayton Chipando (Baba Levo) ni diwani wa Kata ya Mwanga Kaskazini katika mkoani Kigoma kupitia chama cha ACT Wazalendo.

Hii ni tafsiri kuwa dunia inaelekea kubadilika kutoka kufuata siasa za mfumo rasmi na kuwaingiza watu ambao hawakuwahi kuwa sehemu ya mfumo huo, lakini wanabebwa na wapigakura wao ambao wameamua kuwachagua kutokana na ushawishi,uwezo na nguvu zao ambazo wamejijengea wenyewe bila kutegemea vyama vya siasa.

Uganda: Nchini Uganda tunaye Mbunge wa jimbo la Kyadondo mashariki, Robert Ssentamu au maarufu kwa jina la Bob Wine ambaye ni mwanamuziki mashuhuri wa miondoko ya dancehall. Bob Wine kwa sasa amekuwa mwiba mchungu kwa utawala wa Rais wa Yoweri Museveni, akiwa anakubalika na kuwavutia maelfu ya vijana ambao wanamuunga mkono. Bob Wine alishinda kiti cha ubunge akiwa mgombea binafsi baada ya kutojiunga na chama chochote.

Kenya: Nchini Kenya mwanamuziki Charles Njagua Kanyi maarufu kwa jina la Jaguar alishinda ubunge wa Starehe jijini Nairobi.

Kanye West ni miongoni mwa wanamuziki ambaye amekuwa akieleza baya kuwa atagombea urais mwaka 2020 nchini Marekani. Lakini swali kubwa linaloibuka sasa ni kama kweli atagombea dhidi ya 'rafiki yake' rais Donald Trump wa chama cha Republican. Orodha ya wanamuziki au wasanii nchini Marekani kuwania urais inaweza kuongezeka kadiri muda unavyokwenda.

Kuibuka kwa Volodymyr Zelensky

Katikati ya mjadala kuhusu nafasi ya wanamuziki, wanasoka,wanamitindo, wachekeshaji kwa ujumla wake, ndipo anaibuka Volodymyr Zelensky huko nchini Ukraine. Huyu ni mchekeshaji ambaye amewavutia maelfu ya vijana na wapigakura nchini humo baada ya kujijenga binafsi kuliko kutegemea nguvu za chama.

Kimsingi Volodymyr Zelensky ambaye alipambana katika duru ya pili ya uchaguzi na mpinzani wake Petro Poroshenko, anakuwa miongoni mwa waburudishaji wanaoteka siasa duniani.

Mchekeshaji Volodymyr Zelensky ndiye mshindi wa kinyang'anyiro cha urais nchini Ukraine. Ushindi wake unatoa ujumbe kwa ulimwengu juu ya mabadiliko ya kisiasa na duniani kutoka siasa za kihafidhina hadi siasa za kisasa ambapo watu waliopo nje ya vyama vya siasa wana ushawishi mkubwa kuliko waliomo ndani ya vyama vya siasa.

Duru za kisiasa zinaonyesha Volodymyr Zelensky hana uzoefui wa kutosha kama walivyo waburudishaji na wanamichezo wengine lakini kukubalika kwake miongoni mwa wananchi wa Ukraine kunaelezewa kama pigo kwa wanasiasa wa vyama.

Volodymyr Zelensky ana umri wa miaka 41 ambaye amekuwa akiigiza kama rais katika filamu maarufu katika runinga nchini humo. Kabla ya ushindi wake katika duru la kwanza la uchaguzi alipata asilimia 30.5 ya kura, dhidi ya 16.6 za rais Petro Poroshenko.

Aidha, mchekeshaji huyo amewashinda wanasiasa wakongwe kama vile waziri mkuu wa zamani Yulia Tymoshenko aliyeshika nafasi ya tatu katika uchaguzi huo akiwa na asilimia 13.2 ya kura katika uwanja mkubwa wa mapambano wa wagombea 39 katika uchaguzi huu wa urais nchini Ukraine.

Kwa mujibu wa Kamusi Elezo Huru, Zelensky alizaliwa Januari 25, 1978 katika mji wa Kryvyi Rih, nchini Ukraine kwa wazazi Wayahudi. Baba yake ni Profesa Oleksandr Zelensky na Mama yake ni Rimma Zelenska. Ana shahada ya sheria kutoka Kyiv National Economic University lakini hajawahi kuitumia fani yake. Mwaka 2014 ndio rasmi aliingia kwenye harakati za kisiasa.

Udhaifu wa sera zao na uzoefu

Kwa upande mwingine wanamichezo hawa wamekuwa wakikoslewa kutokuwa na uzoefu kwenye siasa na sera. Watu wanaomkosoa mchekeshaji Zelenskiy ni sawa na ambavyo hapa nchini wasanii wanavyokosolewa kutokana wapinzani wao kutumia uzoefu mdogo kwenye siasa na sera kama kigezo cha kuwapinga. Lakini idadi kuba ya wapigakura imethibitisha kuwa na imani nao, hali ambayo inabomo mfumo wa kisiasa.

Mwanzoni huwa tunaambiwa kuwa wanamichezo hao ni chaguo baya kwa taifa, lakini kadiri muda unavyozidi kwenda mbele tunagundua kuwa wale wanasiasa waliojikita kwenye mfumo wao hawawataki hawa wanasiasa wa kisasa ambao hawajapitia vyama vyao. Ni tatizo la wahafidhina, sio hawana wanamuziki,wanamitindo,wacheza filamu na wanasoka. Dunia inazidi kubadilika, tuendako wanasiasa kutoka kwenye michezo na burudani watazidi kutamba bila kutegemea vyama vya siasa.