Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo Uganda, Rwanda: Mfanyabiashara wa Uganda aishitaki Rwanda
Mfanyabiashara mmoja wa Uganda amefikisha ombi la kuishitaki Rwanda katika Mahakama ya haki ya Afrika Mashariki kwa tuhuma za kuvunja mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ombi la mfanyabiashara huyo lilifikishwa ofisi ya Mahakama ya Afrika Mashariki mjini Kampala siku ya Ijumaa, na tayari limewasilishwa rasmi kwa mkuu wa Sheria wa Rwanda.
Wakili wa mfanyabiashara huyo Kalali Steven, anadai kuwa mteja wake ameghabishwa na hatua ya Rwanda ya kuzuia bidhaa na wafanyabiashara kutoka Uganda kuvuka na kuingia vituo vya Cyanika, Gatuna na Mirama Hills nchini Rwanda.
Akizungumza na BBC wakili Kalali Steven ,amesema kimsingi wanachokitafuta katika mahakama ya haki ya Afrika Mashariki iliyo na makao yake mjini Arusha sio fidia kwa sasa, bali ni fasiri ya uhalali wa hatua ya Rwanda kuzuia bidhaa na wafanyibiashara kutoka Uganda kuanzia tarehe 27 Februari mwaka huu kuingia Rwanda.
''Uamuzi wa kuzuia bidhaa za Uganda na wafanyibiashara au wachuuzi wasiingie Jamhuri ya Rwanda unavunja thamani za kimsingi za uasisi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na mkataba uliotiwa sahihi'',alisema wakili huyo.
Ombi la mashtaka linataja vipengee karibu kumi vya mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambavyo linatuhumu kuvunjwa na Rwanda kwa kuwekea vizuizi bidhaa na wafanyibiashara wa Uganda kuingia Rwanda.
Mshitakiwa katika ombi hilo ni mwanasheria mkuu wa Rwanda na anasiku 14 kujibu na mshitaki ni mfanyibiashara Kalali Steven.
''Tulikua na mteja mmoja kwa jina Kaziba Amos aliyekuwa na samaki na na mazao mengine ambayo yalioza. Pia baadhi ya madereva walituambia ya kwamba nyakati fulani maafisa maafisa wa Rwanda waliyaruhusu magari kutoka Kenya na Tanzania kupita, lakini yale ambayo hasa yalikua na nambari za Uganda yalizuiliwa na kuambiwa kuwa ni amri kutoka juu'' aliongeza Bw. Kalali
Inasadikiwa kuwa katika mfumo wa Rwanda hakuna amri ya juu zaidi kumshinda Rais Paul Kagame.
Katika kikao kilichotangazwa moja kwa moja kwenye televisheni mwezi uliyopita Bw. Kagame aliwaeleza maafisa wa Rwanda kutobuni kisababu kwa mtu yeyote linapokuja suala la kudhibiti mpaka wao na Uganda
''Wale wanaohusika na miundo mbinu, utawala wa kienyeji, uwaniaji na kadhalika fanyeni kile kinachowezekana haraka mruhusu bidhaa na watu hasa wakati huu kwa sababu tatizo lipo hapo lakini pia nimekubali kwamba tunaweza kuwashauri Warwanda wasiende huko'', alisema Rais Kagame.
Hata hivyo mambo bado yamekwama na takwa kuu la wakili Kalali Steven kwa niaba ya wateja wake, ambalo aliwasilisha kwa ubalozi wa Rwanda mjini Kampala siku 14 zilizopita ni Rwanda kuondoa vizuizi mpakani dhidi ya biashara na Uganda.