Utafiti: Uvutaji sigara na kisukari huongeza hatari ya wanawake kupata mshtuko wa moyo

Wanawake wanaovuta sigara, wanaougua kisukari au waliyo na tatizo la shinikizo la damu wako katika hatari ya kupata mshtuko wa moyo.

Kwa mujibu wa utafiti mpya uliyofanywa nchini Uingereza, wananawake wanastahili kupewa ushauri sawa na wanaume na pia kupewa ushauri wa kuachana na uvutaji sigara.

Watafiti wanatoa wito kwa madaktari kusaidia katika harakati ya kuwatambua wanawake waliyo katika hatari ya kupata mshtuko wa moyo.

Hata hivyo watafiti hao wanasema wanaume bado wako katika hatari ya kupata mshtuko wa moyo mara tatu zaidi ya wanawake.

Utafiti huo uliyofanywa na watafiti wa chuo kikuu cha Oxford ulijumuisha karibu watu 500,000 waliyo na miaka kati ya 40-69 ambao wameorodheshwa katika data ya afya ya Uingereza.

Watafiti walibaini kuwa watu, 5,081 waliyofanyiwa uchunguzi walikabiliwa na mshuko wa moyo zaidi ya miaka saba na wengi wao ni wanawake.

Japo hatari ya kupata mshtuko wa moyo kwa wanawake iko chini kuliko wanaume wa miaka yote, kuna baadhi ya sababu zinazowafanya waopi kuwa katika hatari ya kupata mshtuko wa moyo.

Wanawake wanaovuta sigara wako katika hatari ya kupata mshtuko wa moyo kuliko wale ambao hawavuti sigara.

Wanaume wanaovuta sigara wako katika hatari ya kupata mshtuko wa moyo mara mbili zaidi.

Shinikizo la damu linaongeza hatari ya wanawake kupata mshtuko wa moyo kwa 83%.

Utafiti pia umebaini kuwa aina ya kwanza na ya pili ya kisukari zinawaweka wanawake katika hatari ya kupata mshtuko wa moyo kuliko wanaaume

Watafiti wanasema sababu za kibayolojia huenda zikachangia hali hiyo.

Kwa mfano aina ya pili ya kisukari,ambayo mara nyingi inahusishwa na mtindo wa maisha ya mtu binafsi huenda ikaathiri zaidi moyo wa mwanamke kuliko ule wa mwanamume.

Hata hivyo utafiti unasema kuwa wanawake hawana ufahamu kwamba wako katika hatari ya kupata ugonjwa wa moyo na huenda wakawa wanapokea matibabu yasiyofafaa.

Watafiti aidha wanasema wanaume pia huenda wakawa katika hatari ya kupata mshtuko wa moyo lakini ugonjwa huo umechangia pakubwa vifo vya wanawake nchini Uingereza.

Dalili za mshtuko wa moyo

Kwa mujibu wa mtandao wa huduma ya kitaifa ya afya nchini Uingereza mtu anastahili kutafuta ushauri wa kimatibabu akijipata na dalili hizi.

  • Kuumwa na kifua hasa seheku ya katika ya kifua, kujihisi kubanwa kifua hadi unashindwa kupumua vizuri
  • Kuumwa na viungo vya mwili- unahisa kama uchungu unatoka kifuani kuelekea upande wa mkono wa kushoto.
  • Kusikia kisunzi
  • Kutokwa na jasho
  • Kuishiwa na pumzi
  • Kujihisi mgonjwa
  • Kuwa na wasiwasi kupita kiasi
  • Kukohoa au kupumua kwa shida

Japo kuumwa na kifua huwa ni dalili mbaya zaidi, baadhi ya watu huenda wakahisi maumivu kidogo kifuani na katika visa vingine huenda mtu asiumwe na kifua kabisa.

Dalili hizo sana sana zimeelezewa kuwapata wanawake, wazee na watu wanaougua kisukari.

Jinsi ya kuboresha afya ya moyo wako:

  • Wachana na uvutaji sigara
  • Fanya mazoezi
  • Dhibiti uzito wako
  • Kula chakula chenye kiwango cha juu cha ufumwele
  • Punguza mafuta
  • Kula mboga na matunda kila siku.
  • Punguza kiwango cha chumvi
  • Kula samaki
  • Punguza pombe

Dkt Elizabeth Millett, mtafiti mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Afya kutoka chuo Kikuu cha Oxford, amesema ugonjwa wa moyo pia una waathiri wanawake na kwamba hilo linastahili kutiliwa maanani.

"Wanawake wanatakiwa kujua kuwa wako hatarini, lakini licha ya kampeini nyingi kuhusiana na ugonjwa huo bado baadhi yao hawajalitilia maanani.

Ameongezea kuwa siku zijazo idadi ya wanawake wanaofariki kutokana na ugonjwa itakuwa sawa na ya wanaume.