Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Yusaku Maezawa: Elon Musk azindua mtalii kwa kwanza atakayekwenda kwenye Mwezi akitumia chombo cha SpaceX
Kampuni ya tajiri maarufu Elon Musk ya SpaceX imetangaza nani atakuwa abiria wake wa kwanza, mtalii, ambaye atasafirishwa kwenda kuuzunguka Mwezi.
Mtalii huyo atakuwa ni bilionea Mjapani Yusaku Maezawa, 42, ambaye pia ni mjasiriamali na mwenye biashara kubwa ya uuzaji wa mitindo ya mavazi na ubunifu kupitia mtandao.
Mwenyewe ametangaza: "Nimeamua kwenda kwa Mwezi."
Anatarajiwa kusafiri kwa kutumia chombo cha roketi kwa jina Big Falcon Rocket (BFR), ambacho ni chombo cha usafiri wa anga za juu kilichozinduliwa na Bw Musk mwaka 2016.
Hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa binadamu kwenda kwenye Mwezi tangu safari zilizofanywa na wana anga walioabiri chombo cha Apollo 17 cha Shirika la Anga za Juu la Marekani (Nasa) mwaka 1972.
Tangazo kwamba Yusaku atakuwa wa kwanza kufanya ziara hiyo ya kihistoria lilifanywa katika makao makuu ya SpaceX mjini Hawthorne, California, siku ya Jumanne.
Kampuni hiyo imesema safari hiyo itakuwa "hatua kubwa sana katika kuwezesha watu wa kawaida ambao wamekuwa na ndoto ya kusafiri anga za juu wakati mmoja maishani".
Awali kwenye Twitter, Bw Musk alikuwa tayari amedokeza kwamba abiria huyo atakuwa kutoka Japan.
Ni wanadamu 24 pekee ambao wamewahi kusafiri kwenda kwenye Mwezi na wote walikuwa Wamarekani.
Waliokuwa kwenye safari za Apollo 8, 9 na 13 waliuzunguka Mwezi bila kutua.
Hata hivyo, bado haijabainika bilionea huyo atafanya safari yake wakati gani.
Hii ni kutokana na hali kwamba itategemea chombo cha anga za juu ambacho bado hakijaundwa kufikia sasa.
Mwaka 2017, Musk alitangaza kwamba atakuwa akiwatuma watalii wawili, ambao watalipia gharama ya safari hiyo, kwenda kuuzunguka Mwezi.
Mpango huo ulitarajiwa awali kuzinduliwa mapema mwaka huu.
Wakati huo, SpaceX walikusudia kutumia mtambo wa roketi wa kurusha vyombo vya anga za juu kwa jina Falcon Heavy na chombo cha anga za juu chenye kuwabeba wana anga kwa jina Dragon.
Lakini Februari mwaka huu, Bw Musk alisema SpaceX wataangazia kutumia BFR katika safari zake za baadaye zenye kuwabeba binadamu.
BFR haijawahi kurushwa angani lakini Bw Musk ametoa maelezo kadha ya kiufundi kuhusu roketi hiyo yenye kubeba chombo cha anga za juu.
Roketi hiyo inatarajiwa kuwa na urefu wa mita 106 na kipenyo cha mita 9.
Kwa kulinganisha na Falcon Heavy ilikuwa na urefu wa mita 70 na ilikuwa na kitovu cha roketi kilichozungukwa na mitambo miwili ya kuongeza nguvu, kila chombo kikiwa na kipenyo cha mita 3.66.
Jumatatu, Bw Musk alizindua mchoro mpya wa BFR na chombo ambacho kitawabeba abiria kuuzunguka Mwezi.
Mchoro huo ulionekana kuthibitisha kwamba mabadiliko yamefanyiwa chombo hicho, ikiwa ni pamoja na sehemu zinazokaa kama mikia mitatu mikubwa sehemu ya nyuma na sehemu nyeusi ya kukinga dhidi ya jua kwenye sehemu ya chini ya chombo hicho.
Chombo hicho cha BFR kinatarajiwa mwishowe kuwa na uwezo wa kusafirisha vitu vya uzani wa tani 150 hadi kwenye mzingo wa chini wa Dunia.
Uzani huo ni zaidi ya uzani ambao ulibebwa na roketi za US Saturn V zilizotumiwa katika safari za Apollo.
Mwanzilishi huyo wa SpaceX amekuwa akishutumiwa karibuni. Alionekana akivuta sigara akishirikishwa kwenye video ya mtandaoni na mchekeshaji mmoja wa Marekani.
Jumatatu ilibainika kwamba ameshtakiwa kwa kumharibia jina mpiga mbizi mwokoaji wa wavulana waliokwama pangoni Thailand kwa sababu ya kudai mara kadha kwamba yeye ni mtu anayewadhalilisha watoto.
Mpiga mbizi huyo Mwingereza anataka alipwe $75,000 (£57,000) na Musk azuiwe kutoa madai kama hayo siku zijazo.
Hisa za kampuni ya Tesla zimekuwa zikishuka dhamani kwa muda na mjasiriamali huyo aliandika kwenye Twitter kwamba anataka kuifanya kampuni hiyo kuwa ya kibinafsi mwezi mmoja uliopita. Lakini wiki mbili baadaye alibadilisha wazo hilo.
Unaweza kusoma pia: