Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ruth Kamande: Kwa nini Amnesty International wanataka malkia wa urembo gerezani Kenya aondolewe hukumu ya kifo
Shirika la Amnesty International limetoa wito wa kubatilishwa kwa hukumu ya kifo iliyotolewa dhidi ya malkia wa urembo gerezani nchini Kenya Ruth Kamande.
Mwanamke huyo alihukumiwa kifo Alhamisi baada ya kupatikana na kosa la kumuua mpenzi wake miaka mitatu iliyopita katika mtaa wa Buruburu, Nairobi.
Bi Kamande, 25, amekuwa akizuiliwa rumande katika gereza kuu la wanawake la Lang'ata jijini Nairobi ambapo mwaka 2016 aliibuka kuwa malkia wa shindano la urembo lililoandaliwa humo gerezani.
Mkurugenzi mkuu wa Amnesty International nchini Kenya Irungu Houghton amesema mwanamke huyo anafaa kusaidiwa kujirekebisha badala kuhukumiwa kifo.
"Tunasikitika kwamba Kenya inaendelea kutoa adhabu hii katili, isiyo na utu na iliyopitwa na wakati. Hukumu hii ni pigo kwa rekodi nzuri ya Kenya ya kuendelea kubadilisha hukumu za kifo kuwa hukumu za vifungo jela," amesema.
"Hakuna ushahidi wowote wa kuaminika kwamba hukumu ya kifo huwazuia watu kutekeleza uhalifu zaidi ya adhabu za aina nyingine. Hukumu hii ya kifo inafaa kubatilishwa mara moja na Ruth Kamande asaidiwe kurekebisha tabia."
Ingawa huku ya kifo huendelea kutolewa kwa makosa ya mauaji na wizi wa kutumia mabavu nchini Kenya, haijatekelezwa kwa mfungwa yeyote nchini Kenya katika kipindi cha miaka 30.
Rais Uhuru Kenyatta na mtangulizi wake Mwai Kibaki walibadilisha hukumu ya wafungwa wengi waliokuwa wamehukumiwa kunyongwa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita na kuwa vifungo vya maisha jela.
Wafungwa takriban 6,747 wamenufaika kupitia hatua hiyo.
Hukumu ya kifo iliondolewa katika mataifa 139 duniani lakini bado kuna nchi zinazotekeleza hukumu hiyo zikiwemo Marekani, China, Pakistan na Saudi Arabia.
Amnesty wanasema hapana shaka kwamba familia ya marehemu Farid Mohamed ni lazima "itendewe haki" lakini suala kuu wanalopinga ni kutumiwa kwa hukumu ya kifo.
Wamesema nchini Kenya ni kawaida kwa kesi kutoendeshwa kwa njia ya haki na mtu asiye na makosa kujipata amehukumiwa.
Kuna mambo ya kuzingatia pia katika kesi ya Ruth Kamande, wameandika kwenye Twitter: "Alikuwa kijana, aliyekuwa ameathiriwa na wasiwasi na hatari ya kuambukizwa Ukimwi/Virusi Vinavyosababisha Ukimwi. Tangu wakati huo ameonesha nia ya kubadilika akiwa mahabusu. Ingawa haki ni lazima itendeke, hukumu ya kifo si moja ya njia za kufanikisha hilo."
Baadhi ya Wakenya mtandaoni wamekuwa wakikosoa hatua ya Amnesty International kutoa taarifa ya kuomba hukumu dhidi ya Bi Kamande ibadilishwe, wakishangaa iwapo ni kutokana na umaarufu alioupata kwa kuwa Miss Lang'ata Women Prison 2016.
Jaji alisema nini?
Ruth Wanjiku Kamande alipatikana na kosa la kumuua mpenzi wake Farid Mohammed katika mtaa wa Buruburu, Nairobi mnamo tarehe 20 Septemba, 2015.
Jaji Jessie Lessit alisema upande wa mashtaka ulithibitisha kesi hiyo ya mauaji bila shaka yoyote.
Jaji huyo amesema hukumu hiyo inafaa kuwa funzo kwa vijana ambao wanafaa wafahamu kwamba "si vyema kumuua mpenzi wako, ni vyema kujiondokea ukaenda zako."
Wakati wa kukamatwa kwake, mwanamke huyo mwenye miaka 25 sasa alikuwa ndio tu amejiunga na Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) kusomea Uanabiashara, kwa mujibu wa wakili wake.
Ruth Kamande alijitetea vipi?
Mwanamke huyo alikuwa amejitetea kortini na kusema mzozo kati yake na marehemu ulizidi baada yake kugundua kadi ya hospitali iliyoashiria kwamba Mohammed alikuwa anapokea matibabu ya Ukimwi.
Alisema alimkaripia kumwuliza ukweli kuhusu hilo na kwa mujibu wake, marehemu alimwambia wakati huo kwamba heri wafe wote kuliko hali yake ya Ukimwi itambulike hadharani.
Bi Kamande anasema mzozo wao ulizidi hata zaidi baada yake kugundua barua za mapenzi kutoka kwa wanawake wengine.
Alisema alimdunga kisu mpenzi wake baada ya kisu cha kutumiwa jikoni kumwangukia wakipigana na hapo akamdunga kisu mara kadha. Anadaiwa kumdunga kisu mpenzi huyo wake mara 22.
Bi Kamande alikuwa ameambia mahakama kwamba marehemu alijaribu pia kumbaka lakini mahakama ilisema uchunguzi wa madaktari ulionyesha hakukuwa na ukweli kuhusu madai hayo.
Mawakili wa Bi Kamande walikuwa wameiomba mahakama kumwonea huruma na kutompa adhabu kali.
Kukumbatia dini
Wakili wake Joyner Okonjo alisema mfungwa huyo alikuwa amejenga "uhusiano wa karibu na Mungu" tangu kuzuiliwa mwaka 2015 na kwamba alikuwa amesilimu na huwa anaomba mara tano kwa siku.
Mahakama iliambiwa kwamba pamoja na hayo ameanza masomo ya dini akiwa gerezani, ishara kwamba amepata funzo akiwa gerezani.
Mahakama iliambiwa kwamba Bi Kamande ni mtoto wake pekee wa mama yake kwa sasa baada ya kaka yake mdogo kufariki.