Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mtandao wa Tinder kutumiwa kuokoa faru
- Author, Anthony Irungu
- Nafasi, BBC Africa, Nairobi
Juhudi za kuokoa faru aina ya 'Northern white Rhino' zimezinduliwa mtandaoni kupitia mtandao wa kijamii wa Tinder.
Ni faru watatu pekee wa aina hiyo waliobaki ulimwenguini.
Watatu hao wanapewa ulinzi mkali wa saa 24 katika hifadhi ya wanyama ya Ol pajeta nchini Kenya.
Faru hao, Sudan - wa kiume, Najin na Fatu - wa kike, ni tasa.
Ol Pajeta imeshirikiana na Tinder kuchangisha dola milioni 9 zitakazofadhili utafiti wa kutafuta mbinu mbadala za kutumia mbegu zao kuzalisha.
Tinder inaongoza ulimwenguni miongoni mwa mitandao ya kijamii inayotumika kutafuta marafiki na wapenzi.
Kupitia kampeni #TheMostEligibleBachelor , Tinder inatumai picha ya Sudan itaonekana katika mataifa 190 ulimwenguni.
Kampeni hiyo inasemekana kuwa njia pekee iliyosalia ya kuokoa faru hao wanaokabiliwa na hatari kubwa ya kuangamia.
Sudan ana umri wa miaka 43, na watafiti wana wasiwasi kwamba huenda akaaga dunia wakati wowote sasa.
Utafiti huo unapania kutafuta mbinu za kisayansi za kuzalisha faru hao, kwa kutumia mbegu zao na faru tofauti aina ya Southern White Rhino.
"tukipata ufadhili, teknolojia hiyo itatuwezesha kufanikisha malengo yetu, na huenda tukapata faru mtoto katika kipindi cha chini ya miaka mitano" Richard Vigne, afisa mkuu mtendaji wa Ol Pajeta ameambia BBC.
Tinder huwa inapatanisha watu milioni 26 kila siku.
"Tinder itaweka picha na maelzo ya Sudan kwenye mtandao huo, na watu wanapopendezwa na picha yake, wataelekezwa kwa mtandao wa kuchangisha pesa" Mathieu Plassard, kutoka Oglivy Africa ameambia BBC.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, wanasayansi wamekuwa wakitafuta mbinu za kutungisha mimba faru wengine kwenye maabara kwa kutumia ovari za faru wa kike.
Iwapo utafiti huo utafanikiwa, itakuwa mara ya kwanza kuhilimisha faru kibandia.
Faru wa kike aina ya 'southern white rhino' atatumika kubeba mimba iliyotungwa kwa kutumia mbegu za faru aina ya 'northern White Rhino'