Serikali ya Burundi imesimamisha shughuli za mashirika 130 yasiokuwa ya kiserikali 'NGO,s' nchini mwake

Serikali ya Burundi imechukua uamzi wa kusimamisha mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayohudumia nchini humo.

Shughuli za mashirika hayo zimepigwa marufuku katika kipindi cha miezi mitatu kwa madai kwamba mashirika hayo yameshindwa kuheshimu sheria za Burundi na kukiuka wajibu wake .

Burundi imeorodhesha mashirika yasiokuwa ya kiserikali zaidi ya 130 na sehemu kubwa ya mashirika hayo ya NGOs ni kutoka mataifa ya magharibu hususan nchi za Muungano wa Ulaya.

Kutoka Bujumbura, mwandishi wetu Ramadhani Kibuga anasema uamuzi huo wa kusimamisha mashirika yasokuwa ya serikali umechukuliwa na Baraza la kitaifa la Usalama katika kikao kilichoongozwa na rais wa Burundi Pierre Nkurunzinza.

Baraza hilo linasema mashirika hayo hayakuzingatia sheria zinazoyahusu kama alivyosema Katibu mtendaji wa baraza la kitaifa la usalama Meja jenerali Silas Ntigurigwa alieleza,

"Baraza Kuu la usalama limechunguza utendaji kazi wa mashirika yasiokuwa ya kiserikali na kugundua sehemu kubwa ya mashirika hayo hayakuzingatia wajibu wake na sheria .

Ndio maana baraza kuu la usalama limechukua hatua ya kusimamisha kwa muda shughuli za mashirika hayo katika kipindi cha miezi sita kuanzia tarehe mosi oktoba mwaka huu".

Katika taarifa hiyo , Baraza hilo halikueleza bayana ni masharika yapi yameshindwa kwenye wajibu wake lakini Msemaji wa rais kwenye mazungumzo na Vyombo vya habari Jean Claude Karegwa amebainisha baadhi ya makosa ya mashirika hayo.

"Kuna baadhi ya mashirika yanayoeneza mafunzo ya ndoa za jinsia moja wanaume kwa wanaume na wanawake kwa wanawake, yote hayo tunayajuwa.

Hii ni kinyume cha sheria. Kuna mashirika yanayotumiwa katika kuchochea vita ili kampuni zinazofanya biashara ya silaha zipate soko ya silaha hizo,

kuna mengine yanayotumiwa kuzagaza maradhi ili kampuni zinazotengeneza madawa zipate soko ya madawa hayo,

kuna na mengine yanayotumiwa kuchochea ghasia na vurumai katika nchi mbalimbali ili nchi hizo zisambaratike na hivyo kampuni za ujenzi zipate soko wakati wa ukarabati".

Mbali na sababu hizo, tayari mapema mwezi huu, Baraza la Seneti lilikemea vikali mashirika hayo yasiokuwa ya kiserikali na kuyashinikiza kubadili mfumo wa kuwaajiri wafanyakazi kwa kuzingatia uwakilishi wa makabila sawa na maagizo ya katiba kwa asilimia 60 kwa Wahutu na asilimia 40 kwa watutsi.

Serikali katika taarifa yake imesema mashirika hayo yasiokuwa ya kiserikali yataruhusiwa tena kufanya kazi baada ya kuchunguzwa na kila shirika kukiri na kuyafanyia kazi mapungufu yake.

Wizara ya mambo ya ndani imeorodhesha zaidi ya mashirika yasiokuwa ya kiserikali 'NGO,s 130' na sehemu kubwa ni kutoka mataifa ya Muungano wa Ulaya pamoja na Marekani.

Wadadisi wa siasa za Burundi wanaona hatua hii kama mwendelezo wa mvutano kati ya Muungano wa Ulaya na Serikali ya Burundi baada ya Shirika hilo kuichukulia Burundi vikwazo kwa madai ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu.